Thursday, July 31, 2008

Simulizi ya Mtoto wa Marehemu Chacha Wangwe

Watoto watu wa marehemu wakiongozwa na mkubwa wao Zakayo Chacha (18), waliezea kuhuzunishwa kwao, juu ya kifo cha mzazi wao wa kiume.
Kwa mujibu wa Zakayo kifo cha baba yao kimetokea wakati mama yao yuko Dar es Salaam. Katika simulizi zake, mtoto huyo alisema kabla ya kifo chake, baba yake alikuwa anasumbuliwa na malaria.
"Tuliondoka naye Dar es Salaam Alhamisi iliyopita, akiwa na makusudio ya kuja kuwasilisha bungeni hoja yake binafsi kuhusu mambo ya Tarime," alisema.
Alisema kwa mujibu wa maelezo ya baba yake, hoja hiyo alitarajia kuiwasilisha Ijumaa, lakini alikosa nafasi. "Lakini kuanzia Ijumaa jioni baba alikuwa anajisikia vibaya, akanywa dawa, pia Jumamosi. Jumapili usiku alitueleza kuwa alikuwa hajisikii vizuri, akaniambia nimtafutie dawa (Panadol), nikatafuta lakini sikupata," alisema kijana huyo huku akionesha masikitiko makubwa.
Alisema aliwasiliana na mama yake kwa njia ya simu kumweleza kuhusu hali ya marehemu na kutoonekana kwa dawa zilizokuwa zimehifadhiwa kabatini. Bw. Chacha alisema baadaye, mama yake alimshauri aende kununua dawa hizo katika duka la jirani na kwamba alipokwenda, duka lilikuwa limefungwa kwa kuwa ilikuwa usiku wa manane. Alisema hata hivyo, muuzaji wa duka hilo alikubali kuwapa dawa alizokuwa amezihifadhi kwa matumizi binafsi. Alisema baada ya kunywa dawa hizo, alilala usingizi mzito," alisema.
Mtoto huyo alisema ilipofika saa 11 alfajiri mtu aliyetamtaja kuwa ni Bw. Deus Malya, ambaye ni rafiki wa marehemu, alikwenda katika makazi hayo na kumtaka marehemu waondoke. "Nilimgongea sana mlango wa chumba chake, hakujibu baadaye nikampigia simu akajibu na baadaye wakaondoka na kurudi," alisema.
Alisema juzi marehemu aliamka akiwa amebanwa na mafua makali na kwamba kwa kumwona akiwa katika hali hiyo, alisihi baba yake apumzike badala ya kwenda bungeni. "Lakini alinijibu kuwa hoja yake ilikuwa ni ya muhimu sana na kwa hiyo lazima aende kuiwasilisha, akaondoka lakini pia nilimshauri apitie hospitalini," alisema Zakayo.
Alisema baadaye baba yake alirejea nyumbani na kumweleza kuwa hoja yake imeshindikana kuwasilishwa. Kwa mujibu wa kijana huyo, marehemu Wangwe pia alimwambia kuwa alipitia hospitalini ambako alipimwa na kukutwa na wadudu watatu wa malaria na kwamba alipewa dawa za mseto ili azitumie.
"Baadaye tulimka ale chakula halafu apumzike, akasema hajisikii kula, lakini alikuwa ameleta matunda akataka tumtengenezee matunda ambayo alisema angeweza kula," alisema. Bw. Chacha alisema baada ya muda, alimpa baba yake dawa za mseto na kumtaka apumzike na kwamba alipokwenda kumjulia hali alikumtaka anakoroma.
"Saa 11 jioni alikuja Deus na kumtaka baba waondoke, lakini kabla hawajaondoka kuelekea Dar es Salaam, nilimweleza Deus kuhusu hali ya gari. "Gari lilikuwa na matatizo nati za matairi ya mbele zilikuwa zimelegea tukajitahidi kuzifunga upya. Baada ya hapo nililijaribu lakini ghafla nati zilichomoka, jambo ambalo kwa kweli nilisema lilikuwa la hatari kama wangesafiri nalo," alinena.
Alisema baadaye alimpa taarifa baba yake ambaye alimshukuru na kumtaka yeye na Deus wakashughulikie gari hilo, ili liwe imara kwa kusafiria. "Gari lilitengenezwa na wakaondoka likiwa linaendeshwa na Deus. Lakini baada ya muda, baba alinipigia siku kuwa gari limewaharibikia Ihumwa na kwamba wanarejea mjini kwenda kulitengeneza. Nikawa nawatafuta sikuwapata.
"Saa mbili usiku nilichukua simu nikaiweka kwenye chaji na baada ya muda, nilipokea simu kutoka kwa mama akiniarifu kuwa baba amepata ajali na amekufa," alisema kijana huyo.
Alisema baada ya taarifa hiyo, alipiga simu ya baba yake ambayo ilipokewa na Deus na kwamba alimuuliza kuhusu habari za kifo cha baba yake, Deus alimjibu kuwa wao walikuwa wamejeruhiwa na walikuwa wanapata matibabu.
Kwa mujibu wa Zakayo, mama yake alipata taarifa hizo kupitia Polisi. Mmoja wa waandishi wa habari hii aliyefika katika chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Mkoa Dodoma jana, alishangaa kuushuhudia mwili wa mbunge huyo ukiwa na majeraha kichwani na mwili mwingine ukiwa shwari.
Hata hivyo alishuhudia damu nyingi kwa imeganda usoni ingawa alimshuhudia Bw. Malya akiwa hana jeraha lolote kunwa la kutisha hasa ikizingatiwa jinsi gari lilivyoharibika. Hadi tunakwenda mitamboni bado hakukuwa na taarifa yoyote ya uchunguzi uliofanywa na wataalamu kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Polisi, Hospitali ya Mkoa Dodoma, ndugu wa marehemu na mwakilishi wa wabunge iliyokuwa imetolewa.
Watoto wengine wawili waliokuwapo katika makazi yao ni Bob na Abdunedo Chacha.

0 comments:

About This Blog

Blog Archive

Waliotembelea ukurasa huu

free counter

  © The Professional Template Under Dullonet Tanzania @ 2008

Back to TOP