Friday, October 3, 2008

Majina ya watoto waliofariki Tabora yatajwa

wahudumu wa hospitali ya kitete wakihudumia maiti za watoo waliofariki kwa kukosa hewa

Baadhi ya ndugu na jamaa wakiwa nje ya hospitali ya mkoa wa Tabora ya Kitete wakisubiri kwenda kutambua maiti za watoto waliofariki katika ukumbi wa Disco mjini tabora

Baadhi ya maiti za watoto waliofariki katika ukumbi wa Disco Mjini Tabora zikiwa zimelazwa katika chumba cha maiti tayari kutambuliwa na ndugu zao
Na Mwandishi wetu , Tabora

MAJINA ya watoto 19 waliokufa kwa kukosa hewa katika ukumbi wa disko mjini hapa, wakati wa kusherehekea sikukuu ya Idd el-Fitri juzi, yametajwa. Wakati majina hayo yakitajwa, Rais Jakaya Kikwete, ametuma rambirambi kwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora na wazazi wa watoto hao.
Watoto hao walianguka baada ya ukumbi wa Bubbles Night Club na Oneten Disko Teck, katika maghorofa ya Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), kutokuwa na hewa ya kutosha, hivyo kusababisha vifo na wengine kujeruhiwa. Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Abeid Mwinyimsa, alisema tukio hilo limeshitua wengi na kwamba limeleta hali ya fadhaa kwa wazazi na walezi.
Aliwataja watoto waliopoteza maisha katika tukio hilo kuwa Veronica Maningu, Beatrice Makelele, Jacob Gerald, Salma Hamis, Hadija Waziri, Rehema Moyo, Seleman Idd, Mrisho Seleman, Abdallah Rehani na Agatha Maningu. Wengine waliopoteza maisha ni Paulina Emmanuel, Ramla Yenga, Mohamed Kapaya, Habiba Shaaban, Donald Kasela, Mwanahamisi Waziri, Philipo Haule, Ashura Jamal na Yassin Rashid.
Mwinyimsa aliwataja watoto waliozimia na kulazwa katika hospitali ya mkoa wa Tabora ya Kitete kwa matibabu kuwa, Sakina Ali, Daudi Chape, Shufaa Azan, Naomi Joseph, Amani Emilian, Jumanne Mashaka, Kulwa Iddi, Msimu Rehani, Bahati Hamisi na Bertha Maneno.
Wengine waliolazwa ni Asia Mohamed, Mwami Masumbuko, Shida Kassim, Kenea Masudi, Agness Kasele, Josephine Julius, Tatu Hamad na Ramadhani Idd.
Akizungumza kwa njia ya simu , Kaimu Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Tabora, Daudi Siasa alisema watoto 10 waliruhusiwa kutoka hospitalini jana, huku sita wakiendelea na matibabu. Kutokana na tukio hilo, Mwinyimsa alisema serikali kupitia vyombo vya usalama, imeanza kuchukua hatua madhubuti baada ya kuwakamata watu waliokuwa wakipiga disko katika kumbi za Bubbles na Oneten katika jengo la NSSF yalikotokea maafa hayo.
Mbali na kukamatwa kwa watu hao, alisema serikali imeunda tume itakayofanya kazi kwa siku saba kuchunguza chanzo cha tatizo hilo.
Alisema tume hiyo itahusisha watu kutoka idara za ujenzi, Jeshi la Polisi na usalama wa taifa na inatakiwa kuwasilisha taarifa wiki ijayo.
Mwinyimsa alisema serikali itagharamia maziko ya watoto hao, na kutoa ubani wa sh. 50,000 kwa kila mzazi, ikiwa ni pamoja na kupendekeza watoto hao wazikwe mahali pamoja kwa ajili ya kuweka kumbukumbu rasmi.
Kwa mujibu wa watoto walionusurika katika ajali hiyo ndani ya kumbi hizo za starehe zilizo katika eneo moja, kulikuwa na joto kali na kulikuwa na harufu mbaya. Walisema hali hiyo ilisababisha takriban watoto 50 kuanguka, ambapo 19 walikufa.
Katika hatua nyingine, Rais Kikwete ametuma rambirambi na kutuma ujumbe maalumu utakaoongoza shughuli za maziko zinazotarajiwa kufanyika mjini Tabora. Ujumbe huo utaoongozwa na Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana, Profesa Juma Kapuya. Rais alisema amepokea kwa mshituko mkubwa habari za vifo vya watoto hao na amehuzunishwa na kusikitishwa na msiba huo.
“Nimepokea kwa mshituko mkubwa, huzuni nyingi na masikitiko yasiyokuwa na kifani habari za vifo vya watoto hao wasiokuwa na hatia, ambao walikuwa wanasherehekea sikukuu ya Idd el Fitri kama tulivyokuwa tunafanya sisi sote,” alisema Rais. Aliongeza: “Mawazo yangu yote yako kwa wazazi na wanafamilia wa watoto hao katika kipindi hiki kigumu cha huzuni, majonzi na msiba mkubwa.
Tunawaombea kwa Mwenyeji Mungu waweze kuwa na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu”. Rais Kikwete alisema ni matarajio yake kuwa, vyombo vya sheria vitachunguza kikamilifu na ipasavyo vifo vya watoto hao na kuchukua hatua zinazostahili.

0 comments:

About This Blog

Blog Archive

Waliotembelea ukurasa huu

free counter

  © The Professional Template Under Dullonet Tanzania @ 2008

Back to TOP